Ubalozi Wa Marekani Wahitimisha Programu Ya Kiingereza Moshi

Moshi, TANZANIA. Septemba 18, 2018, wanafunzi 40 wameshiriki katika mahafali ya Programu ya Kiingereza iliyoandaliwa na Ubalozi wa Marekani katika chuo cha Kilimanjaro Information and Technology College (KIT – Moshi) kwa wanafunzi wa kidato cha tatu na nne. Wanafunzi hao, wakiwemo 22 wa kiume na wa kike 18, wamemaliza vizuri mafunzo yao ya miaka miwili ambapo walikuwa wakihudhuria mafunzo ya Kiingereza mara mbili kwa wiki baada ya masomo ya kawaida katika chuo cha KIT.  Hawa wanafunzi ni kundi la pili la washiriki mjini Moshi. Serikali ya Marekani pia inafadhili programu nyingine nne kama hii huko Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza; huko Unguja kwa kushirikiana na wahitimu wa mafunzo mbalimbali yaliyofadhiliwa na Serikali ya Marekani (ZAUSSA); kwa Dar es Salaam katika shule ya Jomak; na huko Tanga yakiendeshwa na Tanga Initiative & Mindset Organization (TIMO).  Ubalozi wa Marekani utaanzisha programu zaidi za Kiingereza huko Mbeya, Mtwara na Pemba. Madarasa yataanza Januari 2019.

Afisa wa Ubalozi wa Marekani anayesimamia ufundishaji wa Kiingereza kanda ya Afika Mashariki na Kati George Chinnery aliwasifu wanafunzi wa programu ya Kiingereza kwa kujitolea kwao. “Kupitia programu hii ya Kiingereza, mmenufaika zaidi mbali ya umahiri wenu katika lugha ya Kiingereza. Mmekuwa viongozi katika jamii na mfano miongoni mwa jumuiya zenu.” Katika mahafali hayo, wanafunzi walionyesha kazi walizofanya darasani kwa Kiingereza, zikigusia miradi ya huduma kwa jamii wakati wa ushiriki wao katika programu hiyo.

Programu ya Kiingereza hutoa mafunzo ya miaka miwili ya Kiingereza kwa vijana mahiri wenye umri wa kuanzia miaka 13 hadi 25 kupitia mafunzo ya kina baada ya masomo ya kawaida shuleni.  Programu ya Kiingereza huwapa washiriki ujuzi katika lugha ambayo huwasaidia kupata kazi bora na fursa za kujiendeleza kielimu.  Washiriki pia hupata uwezo wa kuwania nafasi za kimasomo nchini Marekani.  Programu hii ilianza mwaka 2004, zaidi ya wanafunzi 300 kutoka Tanzania na wanafunzi 100,000 kutoka nchi 85 duniani kote wameshiriki katika programu hii.  Kwa taarifa zaidi, tembelea: https://americanenglish.state.gov/.