Ubalozi wa Marekani watoa magari kwa ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Dar es Salaam – Serikali ya Marekani kupitia programu ya Boresha Afya inayofadhiliwa na Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) imetoa magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Magari haya yatatumiwa na Timu za Menejimenti ya Afya za mikoa ya Lindi na Mtwara kusaidia shughuli za ufuatiliaji wa miradi ya kudhibiti VVU, uzazi wa mpango, kifua kikuu, malaria, lishe, jinsia, ustawi wa jamii na miradi mingine inayohusu afya katika mikoa hiyo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya magari hayo, Kaimu Mkurugenzi wa USAID nchini, David Thompson, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa dhamira yake ya dhati ya kuboresha afya za Watanzania wote. Kaimu Mkurugenzi Thompson alisema, “Kupitia msaada huu, Serikali ya Marekani inaunga mkono na kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuinua upatikanaji wa huduma bora za afya zilizo toshelevu na jumuishi kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara, hasa ikiwalenga wanawake na vijana.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Suleiman Jaffo alielezea shukrani za Serikali ya Tanzania kwa ubia imara kati ya watu wa Marekani na watu wa Tanzania katika miradi ya afya.

 

Kuhusu Programu ya USAID wa Boresha Afya katika Kanda ya Kusini

Programu ya USAID ya Boresha Afya katika Kanda ya Kusini inafadhiliwa na Serikali ya Marekani  kupitia USAID. Programu hii inaendeshwa na Kampuni ya Ushauri ya Deloitte Consulting Limited katika halmashauri zipatazo 43 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma  kwa ushirikiano wa kitaalamu na shirika la Family Health International (FHI360), taasisi ya EngenderHealth na Taasisi ya Menejimenti na Maendeleo ya Afya (Management and Development for Health). Lengo la programu ya Boresha Afya katika Kanda ya Kusini ni kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma bora za afya zilizo toshelevu na jumuishi kwa jamii zinazohudumiwa, hususan, kwa wanawake na vijana tukilenga zaidi huduma kwa akinamama wajawazito, huduma kwa akinamama baada ya kujifungua na watoto wachanga, watoto, afya ya uzazi na lishe.