Flag

An official website of the United States government

Ubalozi wa Marekani wazindua Kongamano la Kwanza la Kikanda la Wanawake Wajasiriamali linalofanyika Tanzania
4 MINUTE READ
Julai 11, 2023

Jumanne, tarehe 11 Julai, 2023, jijini Dar es Salaam, Balozi Michael Battle na Mwakilishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Afisa Biashara Mwandamizi Rashid Kilambo, kwa pamoja, walizindua Kongamano la wahitimu wa Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali Wanawake (Academy for Women Entrepreneurs – AWE) wa Afrika Mashariki.

 

Kongamano la AWE la Afrika Mashariki, linalofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 13 Julai, linawakutanisha wanawake wajasiriamali na viongozi wa biashara120 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, na Rwanda. Wakati wa Kongamano, washiriki walibadilishana ujuzi na uzoefu wao na kuinua uwezo na kujenga mitandao kwa ajili kuimarisha, kukuza ubunifu na uendelevu wa biashara zao. Kongamano hili linakusudia kutumia ujuzi mkubwa wa kibiashara na teknolojia ya Marekani kuwajengea uwezo na kuwezesha wanawake wajasiriamali kutoka Afrika Mashariki kujenga ushirikiano na mitandao imara miongoni mwao. Viongozi wa biashara wa Kimarekani na Kitanzania watawaongoza washiriki kujadili mada mbalimbali kama vile matumizi ya teknolojia kukuza biashara, kujenga biashara ili iwe endelevu na kutafuwa wawekezaji na masoko.

 

Katika hotuba yake, Balozi Michael Battle alisema kuwa toka kuzinduliwa kwake mwaka 2019, AWE imewajengea uwezo wanawake wajasiriamali 25,000 duniani kote. Kutoka kuinua kipato kwa wazalishaji wadogo wadogo kupitia utafutaji masoko kidijitali hadi kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi, wahitimu wa AWE wameonyesha umuhimu wa kuwekeza katika biashara zinazoongozwa na kuendeshwa na wanawake ili kuwa na ukuaji endelevu katika kanda yote ya Afrika Mashariki.

 

AWE ni programu ya Serikali ya Marekani inayolenga kukuza uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake ikilenga kuwasaidia wanawake milioni 50 duniani kote kufikia upeo wao kiuchumi.  AWE imedhamiria kwa dhati kuwapa wanawake ujuzi, kuwajengea mitandao na kuwapa fursa wanazohitaji ili kugeuza mawazo yao ya kibiashara kuwa biashara halisi. Hadi hivi leo programu ya AWE nchini Tanzania kwa kushirikiana na SELFINA imewajengea uwezo zaidi ya wanawake 150 kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kufikia upeo wa mafanikio yao kibiashara.

 

Afisa Biashara Mwandamizi Kilambo alisisitiza, “programu ya AWE imewanufaisha wanawake wengi wajasiriamali, ikiwapatia fursa ya elimu na kujifunza kutoka kwa waliowatangulia.  Ninaamini elimu ni ufunguo wa kuwanyanyua wanawake na kuwapatia fursa sawa katika uwanja uliowekwa sawa kwa wote. Natarajia kusikia zaidi kuhusu matokeo ya Kongamano hili na jinsi wanawake wajasiriamali wa Kitanzania wanaweza kuendelea kukuza biashara zao na kutengeneza njia kwa wanawake wengi zaidi kushiriki na kupata mafanikio ya kiuchumi.”

 

Mshiriki wa AWE, Lightness Salema, ambaye ni mwanzilishi wa Kampuni iitwayo Dream Developers LTD ya jijini Dar es Salaam, alisema, “AWE imenipa ujuzi niliokuwa nauhitaji sana kufikia ndoto yangu ya kukuza uwezo wa wanawake wengine katika jamii yangu kujipatia riziki kupitia biashara yangu ya ufugaji endelevu wa nyuki. Nina shauku kubwa ya kushirikiana na viongozi wengine wa biashara wenye maono na mitazamo kama yangu katika Kongamano hili la AWE la Afrika Mashariki na kujifunza mbinu mbalimbali za kibunifu za kukuza biashara zetu na kuleta mabadiliko katika jamii zetu.”

 

Ubalozi wa Marekani unashirikiana na Selfina kutekeleza programu ya AWE nchini Tanzania. Ikiwa imeanzishwa mwaka 2002 na Dk. Victoria Kisyombe, Selfina ni taasisi ya Kitanzania ya utoaji mikopo midogo midogo iliwalenga zaidi akina mama wajane na wasichana. Katika miaka 19 iliyopita, Selfina imewawezesha kiuchumi zaidi ya wanawake 31,000 kupitia mikopo inayozunguka. Maisha ya zaidi ya watu 300,000 yameguswa kutokana na faida zilizopatikana kutokana na mikopo hiyo. Wanawake sasa ni wamiliki wa biashara zao wenyewe na zaidi ya nafasi za ajira 150,000 zimetengenezwa.