Ujumbe wa Ubalozi wa Marekani kwa Watanzania katika Siku ya Ukimwi Duniani

Na Mratibu wa PEPFAR nchini Brian D. Rettmann | Disemba 1, 2018

Miaka kumi na tano iliyopita pale Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI, au kwa kifupi PEPFAR ilipoanza, nchini Tanzania na mahali pengi duniani, kuwa na VVU ilikuwa sawa na hukumu ya kifo. Leo hii, tupo karibu zaidi kulidhibiti janga hili  kuliko ilivyowahi kuwa wakati mwingine wowote.

Katika kipindi cha miaka 15, Serikali ya Marekani imetoa zaidi ya shilingi za Kitanzania trilioni 180 duniani kote ili kuokoa maisha ya watu milioni 16. Hapa nchini Tanzania, Serikali ya Marekani imetoa shilingi trilioni 9 kusaidia ununuzi wa vifaa vya kupimia VVU, watoa huduma za afya, huduma za ushauri nasaha na – muhimu zaidi – dawa za kufubaza VVU zinazotolewa bure kwa takriban Watanzania milioni moja.

Toka kuanza kwa PEPFAR, ukarimu wa watu wa Marekani  umewezesha kupungua kwa kiwango cha vifo vinavyotokana na UKIMWI kwa asilimia 70 na kupungua kwa kiwango cha maambukizi mapya ya virusi hivyo kwa zaidi ya nusu. Hivyo zaidi ya maambukizi mapya milioni moja  na karibu vifo 700,000 vimezuiwa.

Ni lazima tusherehekee mafanikio haya. Lakini ni lazima pia tuendelee kukumbuka kuwa bado kazi kubwa inahitajika kufanyika katika kukabiliana na VVU na UKIMWI nchini Tanzania.  Karibu nusu ya Watanzania wote wanaoishi na VVU hawajui kama wameambukizwa virusi hivyo na hawawezi kupata matibabu yatakayoweza kuokoa maisha yao.  Kuyahimiza makundi ya watu walio kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizo, ikiwa ni pamoja na wanaume, vijana, watumiaji wa madawa ya kulevya na wafanyabiashara za ngono kwenda kupima na kujua hali zao za afya ni muhimu sana katika kukabiliana na VVU na UKIMWI.

Hata hivyo, bado unyanyapaa na ubaguzi unaendelea, iwe ni kwa kauli za chuki zinazotolewa hadharani na viongozi wa kisiasa, unyanyaswaji na hata kukamatwa  kwa makundi ya watu hao walio katika hatari zaidi ya kuambukizwa. Lengo la kutokomeza kabisa janga la VVU nchini Tanzania linaweza kabisa kufikiwa. Lakini halitaweza kufikiwa iwapo vitendo hivi vinavyokwaza jitihada za kufikia azma hiyo vitaendelea.

Kwa pamoja, lengo letu liwe ni kuongeza jitihada za kuwakinga watu wasiambukizwe VVU na kuhakikisha kuwa kila mtu anapima na kujua hali yake ya afya ili wale wanaoishi na VVU waweze kupatiwa matibabu yatakayookoa maisha yao.  Tupo tayari kusaidia kuanzishwa kwa sera itakayowawezesha watu nchini Tanzania kujipima wenyewe VVU (HIV self-testing policy). Kizazi kisicho na UKIMWI kinawezekana.

Tunahitaji kuwapongeza na kujivunia kila mtu anayepima VVU, kwa sababu mtu anapochagua kufanya hivyo, anakuwa amechagua uamuzi mzuri katika kulinda afya yake mwenyewe, afya ya familia na afya ya jamii yake kwa ujumla.

Pale mtu anapotumia dawa za kufubaza VVU, hawezi tena kuwaambukiza watu wengine virusi hivyo. Kwa maneno mengine, kwa kuchagua kupima na kuanza matibabu, watu huboresha sio tu afya zao wenyewe, bali pia afya za familia na jamii zao.

Je unajua hali yako? Kumbuka, kupima ni sawa na kuondoa kitambaa kilichokuwa kimekufunika macho. Kupima hakutabadilisha hali yako kama umeambukizwa au la. Lakini kupima ni hatua ya kwanza ya kuishi maisha mazuri huku ukiendelea na shughuli zako kama kawaida, na kusimamisha kuenea kwa VVU kwa wengine.

Wahimize wengine pia wajue hali zao. Ongea  kuhusu VVU na marafiki, viongozi wako wa kiroho na kijamii, familia yako na hata watoa huduma za afya..

Mawasiliano haya ya wazi kuhusu VVU na UKIWMI ni hatua muhimu ya mwanzo katika safari yetu ya kufikia lengo na kutokuwa kabisa na maambukizi mapya, yaani kuwa na kiwango sifuri cha maambukizi, kwa sababu ili uweze kumfikia na kumsaidia kila mmoja ambaye pengine anaogopa kwenda kupima, ni lazima tuwe na kiwango sifuri cha unyanyapaa.

Kuna nchi 13 duniani ambazo zipo katika mwelekeo mzuri wa kutokomeza kabisa tishio la VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2020. Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi hizo, lakini ipo nyuma ya nchi nyingine katika kanda.  Kazi kubwa zaidi inahitajika kufanyika ili kufikia azma ya kuwa na sifuri tatu, yaani vifo sifuri, maambukizi sifuri na unyanyapaa sifuri. Hivyo hivi leo tunapoadhimisha siku ya UKIMWI Duniani, tujipongeze kwa masafa marefu tulipotoka hadi kufika hapa tulipo na kuazimia kwa dhati kabisa kuhakikisha kuwa Tanzania inaingia katika orodha hiyo.

Marekani inaendelea kuwa mbia wa Tanzania mwenye fahari na mwenye dhamira ya dhati ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wetu jumuishi miongoni mwa watu wa mataifa yetu ili kujenga Tanzania yenye usalama, ustawi na afya kwa Watanzania wote.

Asanteni Sana.