Programu Ya Bahati Nasibu Ya Viza Ya Ukaazi Wa Kudumu Marekani Imeanza

Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam unatangaza kuanza kwa programu ya Bahati Nasibu ya Viza ya Ukaazi wa kudumu Marekani (Diversity Visa Program) kwa mwaka 2018 (DV-2018).  Kila mwaka, kupitia programu hii, Marekani hutoa viza za ukaazi wa kudumu (immigrant visas) zipatazo 55,000 kwa raia wa nchi ambazo kihistoria zina idadi ndogo ya watu wanaohamia Marekani. Mwaliko unatolewa kwa Watanzania wenye sifa kutuma maombi yao katika programu hii ya uhamiaji kabla ya tarehe 7 Novemba 2016.

Tafadhali soma kwa makini na kwa ukamilifu maelekezo ya namna ya kutuma maombi yako katika tovuti maalumu ya Masuala ya Uhamiaji katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inayopatikana katika anuani ifuatayo; www.dvlottery.state.gov.  Maombi ya kupata viza hiyo katika kipindi cha mwaka 2018 (DV-2018) yanapokelewa hivi sasa hadi tarehe 7 Novemba 2016 saa.  Unaweza kutuma ombi lako mara moja tu na kwa njia ya mtandao pekee.  Maombi hayatapokelewa kwa njia ya barua wala kuletwa kwa mkono.

Tafadhali zingatia taarifa muhimu zifuatazo:

  • Hakuna ada yoyote inayotozwa kwa kutuma maombi yako kupitia mtandao. Tafadhali usitume, usilipe wala kuhamishia fedha kwa taasisi au mtu yeyote anayedai anaweza kukusaidia kupata viza hii au kuongeza nafasi yako ya kushinda Bahati nasibu hii.
  • Iwapo utashinda bahati nasibu, utatakiwa tu kulipia ada ya maombi ya viza katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam wakati utakapoitwa kwa ajili ya usaili wa viza. Iwapo kuna mtu yeyote atakayekudai fedha kwa ajili ya kukusaidia kuingia katika Bahati nasibu hii, tafadhali wasiliana na Ubalozi wa Marekani.
  • Kushinda bahati nasibu hii hakukuhakikishii moja kwa moja kupata visa. Iwapo utashinda bahati nasibu bado utahitajika kusailiwa ili kuona kama unakidhi matakwa ya sheria ya Uhamiaji ya Marekani.
  • Unaweza kuwajumuisha watu wa familia yako (mke/mume na watoto wako wa kuwazaa ambao bado hawajaoa au kuolewa walio chini ya miaka 21) katika maombi yako ya Viza hii.  Iwapo utaongeza watu wengine (mbali na hao waliotajwa) maombi yako ya Viza yatakataliwa.  Iwapo mtu yeyote atakuomba ujumuishe watu wengine katika maombi yako ya visa, tafadhali wasiliana na Ubalozi wa Marekani – si lazima utaje jina lako utakapotupatia taarifa hiyo.
  • Orodhesha watu wote wa familia yako (immediate family) katika maombi yako hata kama watu hao wasingependa kuhamia Marekani pamoja nawe. Kushindwa kufanya hivyo kutasababisha wewe kukosa sifa na maombi yako kukataliwa wakati wa usaili wa viza.

Iwapo una maswali zaidi, tafadhali tuma maswali hayo kwa barua pepe ifuatayo; DRSIV@state.gov.