Novemba 23, serikali ya Marekani ilifanya dhifa ya kuadhimisha miaka 60 tangu Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) lilipoanzishwa na Rais John F. Kennedy. Kwa miongo sita, USAID imejenga sifa yake kama kiongozi wa ulimwengu katika maendeleo ya kimataifa kwa kushirikiana na nchi zote ulimwenguni kuimarisha jamii na kuboresha maisha.
Katika zaidi ya nchi 100 duniani kote, timu ya USAID na washirika wanafanya kazi kwa pamoja katika miradi ya maendeleo na ya kibinadamu ambayo huokoa maisha, kupunguza umaskini, kuimarisha utawala wa kidemokrasia, na kuboresha afya, elimu na ustawi wa kiuchumi.
USAID imesaidia Tanzania tangu mwaka 1961. Leo USAID inafanya kazi kwa karibu na watu wa Tanzania, wafanyabiashara, asasi za kiraia na serikali kusaidia vijana wa Kitanzania kuendeleza ustawi wa muda mrefu wa nchi na kujitegemea.
Akizungumza katika hafla hiyo jana, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald J. Wright alisema, “Wakati tunafanya jitihada kuwa na Tanzania inayojitegemea, hakuna nchi iliyo kisiwa lazima tushirikiane pamoja. Kadri ulimwengu wetu unavyounganishwa zaidi, tunakabiliwa na changamoto mpya, za karne ya 21, kama vile mabadiliko ya tabia nchi, vitisho vya teknolojia ya kidijitali, na magonjwa yanayoibuka.”
Balozi aliendelea, “Masuala haya yanaweza tuu kushughulikiwa kwa ushirikiano, kufanya kazi kwa pamoja na kuheshimiana. Ndio maana sisi, watu wa Marekani, na Serikali ya Marekani, tumejitolea kufanya kazi bega kwa bega na wenzetu wa Tanzania katika Serikali, asasi za kiraia, na sekta binafsi ili kukabiliana na changamoto za leo, kwa ajili ya kesho iliyo bora zaidi.
Hakuna ushahidi zaidi ya mawazo haya leo kuliko USAID na juhudi za pamoja za Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na janga la UVIKO-19. Kufikia sasa USAID na Ubalozi wametoa zaidi ya dola za Marekani bilioni 9.8 kupambana na UVIKO-19 katika zaidi ya nchi 120. Nchini Tanzania, Serikali ya Marekani imetoa chanjo zaidi ya milioni 15 na USAID imechangia zaidi ya dola milioni 25 kupambana na janga la UVIKO-19.
Pia akizungumza kwenye hafla hiyo jana, Mkurugenzi mkazi wa USAID Bi. V. Kate Somvongsiri amesema, “Marekani na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu, ambao nina uhakika utaendelea kwa vizazi na vizazi. Tunaamini sana katika kusaidia nchi kote ulimwenguni kuwa na uwezo wa kujitegemea zaidi. Lakini, kujitegemea sio lengo la mwisho. Ulimwengu huu utastawi tu kupitia usaidizi wa pande zote. Kila taifa linakuwa na nguvu zaidi tukisaidiana.”
Kama tulivyo fanya kwa miaka 60, serikali ya Marekani itaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali na watu wa Tanzania ili kuboresha maisha na fursa kwa watu katika nchi zote mbili.