Dodoma – Afisa mwandamizi anayesimamia jitihada za Serikali ya Marekani katika kukabiliana na UVIKO-19 yupo nchini Tanzania katika ziara ya siku tatu kujionea maendeleo yaliyofikiwa na Serikali ya Tanzania katika kutoa chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa watu wake.
Jeremy Konyndyk, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamati Maalumu ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) inayoshughulikia UVIKO-19 yupo nchini Tanzania toka tarehe 16 hadi 18 Mei. Bw. Konyndyk anasimamia maendeleo na utekelezaji wa mipango ya USAID ya kupambana na UVIKO-19, ikijumuisha kusimamia rasilimali zenye thamani ya takriban Dola za Kimarekani billioni 10 zinazotumika kusaidia zaidi ya nchi 100 zinazokabiliana na athari mbaya za janga hili. Aidha, anaongoza shughuli za ushirikiano kati USAID na serikali za kigeni, taasisi wabia, na taasisi maalumu zinazoratibu jitihada za kimataifa za kukabiliana na UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na Gavi/COVAX, Shirika la Afya Duniani na Global Fund. Wasifu: https://www.usaid.gov/who-we-are/organization/jeremy-konyndyk
Mwezi Machi 2022, Tanzania ilichaguliwa kuwa miongoni mwa nchi chache ambazo zingepatiwa fedha kutokana na ongezeko la Dola za Kimarekani Milioni 25 zilizotengwa kwa ajili ya kuongeza kasi ya utoaji chanjo kupitia mpango wa Global VAX, ikiwa ni jitihada za Serikali ya Marekani za kuhakikisha kuwa chanjo dhidi ya UVIKO-19 zinawafikia wale wote wanaotakiwa kuchanjwa. Mtendaji Mkuu wa USAID Samantha Powers alitoa ahadi hii alipokutana na Rais Samia Suluhu Hassan.
Fedha hizi zitasaidia shughuli zinazolenga kuongeza kasi ya utoaji chanjo, ikiwa ni pamoja na kuongoza imani na uhitaji wa chanjo pamoja na kuongeza upatikanaji na vituo vya utoaji wa chanjo hizo. Shughuli zote hizi zinapangwa na kuratibiwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania, kwa mujibu wa mipango ya utoaji chanjo ya Tanzania. Aidha, Serikali ya Tanzania itasaidia kuhakikisha kuwa chanjo zinawafikia watu kwa haraka na kwa usawa. Fedha hizi za ziada kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 25 ni nyongeza juu ya Dola za Kimarekani Milioni 42.1 ambazo Serikali ya Marekani kupitia USAID, Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Maradhi (CDC), Wizara ya Ulinzi na Peace Corps imetoa kwa Tanzania ili kukabiliana na UVIKO -19. Uwekezaji huu unasaidia kukinga, kutibu na kujifunza kuhusu ugonjwa huu.
Hivyo basi, ziara ya Bw. Konyndyk ni katika kutambua hatua kubwa iliyopigwa na Tanzania katika kupambana na UVIKO-19 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na fursa ya kuelewa vyema changamoto na vikwazo vinavyoendelea kuikabili Tanzania inapotekeleza azma yake ya kuchanja asilimia 60 ya watu wake wanaostahili kupata chanjo.
Akiwa nchini Tanzania, Bw. Konyndyk atakutana na maafisa waandamizi wa serikali ya Tanzania katika sekta ya afya pamoja na watoa huduma za afya. Aidha, atatembelea hospitali na vituo vya afya kujionea jitihada zinazofanyika katika utoaji chanjo.