Flag

An official website of the United States government

Mradi wa USAID wa Kuendeleza Mazingira, Uhifadhi, na Utalii Tanzania
4 MINUTE READ
Novemba 13, 2020

DAR ES SALAAM, TANZANIA, Novemba 12, 2020- Leo, mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Kuendeleza Mazingira, Uhifadhi, na Utalii wa Tanzania (PROTECT) ulifanya kikao mtandao kilichorushwa mubashara kusherehekea miaka mitano ya kulinda baioanuai na uchumi unaotokana na utalii.

Hafla hiyo ya kidijitali, “Kuadhimisha USAID PROTECT: Miaka Mitano ya Kuhifadhi Wanyamapori wa Tanzania,” ilionesha mafanikio ya mradi huo, pamoja na jinsi ulivyochangia kupunguza ujangili nchini kwa asilimia 80, kulingana na taarifa za Wizara ya Maliasili na Utalii.

“Kazi nyingi zilizofanywa na USAID PROTECT zitaacha msingi wa kudumu wa uhifadhi nchini Tanzania. Mradi huo umeshirikisha mashirika ya kitaifa na kampuni binafsi zilizopo nchini ili kupata ushawishi na mali zao katika juhudi za uhifadhi. Hii imesababisha kuhifadhiwa kwa zaidi ya hekta 300,000 za maeneo muhimu kibaiolojia na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa cha ujangili na uvuvi usiodhibitiwa.”, alisema Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa USAID, V. Kate Somvongsiri, ambaye alifungua kikao mtandao hicho.

USAID PROTECT, mradi wa miaka mitano wa dola milioni 19.1, ulibuniwa katikati ya janga la ujangili lililoshuhudia Tanzania ikipoteza asilimia 60 ya idadi ya tembo nchini kati ya mwaka 2009 na 2014 pekee. Ili kushughulikia kwa ufanisi tatizo hili, mradi huo ulitumia njia ya ubunifu inayojumuisha sio tu washirika waliozoeleka wa uhifadhi, lakini pia bunge la Tanzania, mahakama, sekta binafsi, na vyombo vya habari. Matokeo yake, Tanzania ilijiandaa vyema kupambana na uhalifu wa wanyamapori katika ngazi zote kupitia sera imara za kuzuia uhalifu wa wanyamapori, uelewa mzuri wa jinsi ya kutambua usafirishaji haramu wa wanyamapori na namna ya kuendesha mashitaka na kesi za uhalifu wa wanyamapori. Mradi huo ulisaidia shughuli mahsusi, kama vile programu za mabadilishano ya uzoefu kikanda na mafunzo ya kupambana na uhalifu huu wenye sura mbalimbali na wa kupangwa.

USAID PROTECT ilishirikiana na Tanzania kuboresha sera juu ya shoroba za wanyamapori kwa kuandaa  Kanuni za Uhifadhi wa Wanyamapori (Shoroba za Wanyamapori, Maeneo ya Mtawanyiko, Maeneo ya Kingo za Maeneo yaliyohifadhiwa na Njia za Uhamaji), pamoja na Mpango Kazi wa Kutathmini vipaumbele vya Shoroba. Hii itahakikisha kwamba shoroba za wanyamapori, maeneo ya mtawanyiko, na maeneo ya kingo za maeneo yaliyohifadhiwa yanapatikana ili kuruhusu wanyama wa porini kutembea kwa uhuru kati ya maeneo yaliyohifadhiwa.

Kama sehemu ya kuandaa wasimamizi wa siku zijazo wa maliasili, USAID PROTECT ilifadhili taasisi tatu za mafunzo ya wanyamapori chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambazo ni Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika – Mweka, Taasisi ya Mafunzo ya Wanyamapori ya Pasiansi, na Kituo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Jamii cha Likuyu Sekamaganga. Kwa kushirikiana na mradi, vyuo viliandaa nyaraka muhimu za taasisi, ikiwa ni pamoja na mipango mikakati, mipango ya biashara, na mikakati ya kutafuta fedha. Nyaraka hizi za msingi ni muhimu kuhakikisha mazingira mazuri ya kujifunza ambayo yanaweza kutoa wahifadhi wa baadae wenye ujuzi,maarifa na wazalendo.

Kujifunza zaidi kuhusu mradi wa USAID PROTECT, tafadhali tembelea: https://www.usaid.gov/documents/1860/promoting-tanzanias-environment-conservation-and-tourism-project-protect