Flag

An official website of the United States government

USAID Yasherehekea Mafanikio ya Mradi wa Lishe Endelevu Uliogharimu Dola Milioni 25 nchini Tanzania
2 MINUTE READ
Septemba 27, 2023

Dodoma – Serikali ya Marekani na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimesherehekea mafanikio ya mradi wa Lishe Endelevu uliolenga kuhakikisha lishe bora inapatikana Tanzania kote. Mpango huu wa serikali ya Marekani wa miaka mitano uliofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) umeleta maendeleo makubwa katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro, na Rukwa.

Lengo kuu la mradi lilikuwa kuimarisha juhudi za kuboresha lishe katika ngazi ya kaya. Kupitia ushirikiano na serikali za mitaa, asasi zisizo za kiserikali na zaidi ya mashirika 300 ya sekta binafsi, mradi umehimiza uzalishaji na upatikanaji wa chakula cha aina mbalimbali kwa kaya na hivyo kusababisha maboresho ya afya yanayoonekana katika maeneo haya.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Kukuza Uchumi ya USAID, Colin Dreizin alisema, “Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018, Mradi wa Lishe Endelevu ulitoa dola milioni 25, na kuhakikisha zaidi ya wanawake milioni 1.6 na watoto milioni 1.2 katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro na Rukwa wanapata huduma muhimu za lishe.”

Katika kipindi hicho, USAID ilifanya kazi kwa karibu na Wizara ya Afya ya Tanzania, Ofisi ya Rais TAMISEMI, na wadau muhimu kama vile Deloitte, AAPH, TMG, na PANITA. Hafla hiyo ilitambua juhudi za Asasi za Kiraia na kuhitimishwa kwa kuzindua Kitabu cha Simulizi za Walengwa cha USAID Lishe Endelevu.

Waziri wa Nchi TAMISEMI Mheshimiwa Mohammed Mchengerwa, alisema, “Leo tumeona mafanikio ya miaka mitano ya mradi wa USAID Lishe Endelevu kupitia kitabu kilichoangazia mikoa hiyo minne. Mradi pia ulisaidia kusimamia uendelevu wa kilimo mseto na ufugaji na hivyo kuongeza upatikanaji wa chakula chenye lishe bora. Tunaishukuru sana USAID kwa kuimarisha eneo la lishe nchini Tanzania.