Flag

An official website of the United States government

Uwekezaji wa Serikali ya Marekani Waimarisha Uwezo wa Maabara zilizo Chini ya Wizara ya Afya
3 MINUTE READ
Novemba 14, 2023

Dar es Salaam – Leo katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUCOHAS), Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI), wamekabidhi vifaa vya maabara. Vifaa hivi vitasaidia kuimarisha uwezo wa wataalamu wa maabara nchini Tanzania katika Upimaji wa vimelea vya malaria kwa ufanisi. Vifaa hivi vyenye thamani zaidi ya dola za kimarekani 488,000, (ambazo ni sawa na Bilioni moja za kitanzania). Vifaa hivi vitapelekwa katika vyuo vya wizara vinavyotoa mafunzo ya kozi ya maabara vilivyopo katika Mikoa sita ambayo ni Mbeya, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Mara, na Singida.

Uwekezaji huu kupitia Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria, PMI, unasaidia moja kwa moja kuendeleza yale yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania kwenye afua zilizothibitishwa kama vile uchunguzi wa kutambua vimelea vya malaria na tiba sahihi kwa wanaogundulika kuwa na vimelea vya malaria; udhibiti wa mbu waenezao malaria kwa njia ya utangamano; ufuatiliaji na tathmini wa mwenendo wa ugonjwa wa Malaria; kutoa elimu, uhamasishaji jamii na uraghbishi; pamoja na utafiti wakati wa utekelezaji.

Hadubini zilizokabidhiwa leo zitasaidia kukuza uwezo wa wataalamu wa maabara kuweza kutambua kwa usahihi vimelea vya Malaria, kwa kuthibitisha uwepo wa vimelea kuwawezesha wataalamu wa afya kuanza matibabu sahihi na kwa haraka, ili kuokoa maisha na kuzuia madhara ya ugonjwa. Aidha, hadubini hizo zitatumika pia kufanya tafiti za kupima ufanisi wa dawa zinazotumika kutibu malaria. Ugunduzi wa mapema wa usugu wa dawa ni muhimu ili kuweza kubadili mikakati ya matibabu kwa wakati na kuzuia usugu usienee, kuhakikisha kuwa dawa za malaria zinazotibu zinaendelea kupatikana kwa watu wote.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa ofisi ya Afya kutoka USAID Tanzania, Bi. Anne Murphy alisema; “Hadubini 133 na vitendanishi vingine vya maabara vilivyotolewa leo vitawezesha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kuimarisha uwezo wa kimaabara katika uchunguzi na kusaidia utoaji matibabu ipasavyo, itakayopelekea kuokoa maisha ya watu na kuzuia madhara ya malaria”.

Serikali ya Marekani inaipongeza serikali ya Tanzania na Wizara ya Afya kwa juhudi zake zilizopelekea kupungua kwa kasi kiwango cha malaria nchini Tanzania kutoka zaidi ya asilimia 14 ya watu mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8 tu mwaka 2022. Serikali ya Marekani inajivunia kuwa sehemu ya mafanikio haya.