Uzinduzi wa AWE Kigoma
Tarehe 6 Februari, Ubalozi wa Marekani ulizindua programu ya Mafunzo kwa Wajasiriamali Wanawake (AWE) mjini Kigoma. AWE ni Programu inayoongozwa na Ikulu ya Marekani ikilenga kuinua maendeleo na ustawi wa wanawake kwa kuwasaidia wanawake wajasiriamali duniani kote. Wanawake 31 wa Kitanzania watashiriki katika mafunzo ya wiki 13 yatakayotolewa kwa njia ya mtandao na kuendeshwa na SELFINA taasisi mbia wa programu ya mabadilishano inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani na yatafanyika katika kumbi za Radio Joy FM.
Programu ya AWE mjini Kigoma ni programu ya nane ya mpango huo kuendeshwa nchini Tanzania ikiwa ni ya kwanza inayojumuisha mafunzo ya Kiingereza. Mikoa mingine iliyofaidika na mafunzo hayo ni Dar es Salaam, Iringa, Zanzibar, Mwanza, Dodoma, Mbeya na Pwani (Bagamoyo). Kupitia programu hii washiriki watajifunza jinsi ya kuandaa mipango ya biashara, kuandaa matangazo ya biashara zao, kuimarisha stadi za kujenga mitandao na kujenga uwezo wa kuongoza na kusimamia biashara zao na hivyo kufanikiwa kama wamiliki wa biashara hizo. Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhingwe na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Kanali Michael Masala Ngayalina na Afisa wa Ubalozi wa Marekani anayeshughulikia Masuala ya Utamaduni Chad Morris.