Flag

An official website of the United States government

Uzinduzi wa Majadiliano ya Kibiashara Kati ya Marekani na Tanzania
Ufunguo wa Kufungua Biashara na Ustawi wenye Manufaa kwa Pande Zote.
6 MINUTE READ
Oktoba 23, 2023

Na Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Michael A. Battle Sr.

Oktoba 22, 2023

 

Alhamisi iliyopita, Marekani na Tanzania zimeingia katika ukurasa mpya wa kimageuzi katika ushirikiano wetu, ambapo Waziri wa Biashara wa Marekani Gina Raimondo na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania Mheshimiwa Dk. Ashatu Kijaji wamesaini hati ya Makubaliano ya kuwa na Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania. Makubaliano haya ya kihistoria yanatokana na ziara yenye mafanikio makubwa ya Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris nchini Tanzania mwanzoni mwa mwaka huu, ziara iliyoweka msingi wa kuinua ukuzaji uchumi, uwekezaji, biashara na ustawi baina ya nchi zetu mbili. Kusainiwa kwa makubaliano haya kunakuja katika kipindi muhimu sana katika uhusiano wetu rasmi na kunaimarisha dhamira yetu ya dhati ya kufanya kazi pamoja ili kuimarisha uhusiano wetu wa kiuchumi kama wabia katika misingi ya kuheshimiana na maadili ya pamoja.

 

Marekani na Tanzania zinaingia katika zama mpya, zama ambazo tunatekeleza vipaumbele vyetu vya ushirikiano wa maendeleo wakati huo huo tukiweka msisitizo zaidi katika kuimarisha uwekezaji na uhusiano wa kibiashara baina ya nchi zetu mbili. Serikali ya Marekani na wawekezaji wa Marekani wanakuja Tanzania, wakiwa tayari kushirikiana kwa namna ambayo itafungua uwezo na fursa kubwa ya kiuchumi ya Tanzania, inayothibitishwa na utajiri wake mkubwa wa rasilimali watu na maliasili zake nyingi.  Tunataka msingi na wigo wa kiuchumi wa Tanzania ukue, na tunaamini katika uwezo wake wa kukua.  Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania ni kielelezo muhimu cha dhamira ya dhati katika kufikia lengo hili. Yatakapotekelezwa, makubaliano haya yatakuwa chachu ya kuongeza biashara kati ya Marekani na Tanzania kwa namna ambayo itawanufaisha moja kwa moja watu wa Tanzania.

 

Wafanyabiashara wa Marekani tayari wanawekeza katika sekta muhimu za uchumi wa Tanzania, lakini hivi sasa uhusiano wa kiuchumi unaelekea kupaa zaidi. Uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na Tanzania ni imara, lakini pia kuna mengi ya kuyafanyia kazi ili uweze kukua zaidi. Mafanikio yaliyofikiwa hivi karibuni kama vile kampuni ya Ward Holdings kuweza kutuma shehena ya korosho zilizobanguliwa katika soko la Marekani, kupokelewa kwa ndege za Boeing kwa ajili ya Air Tanzania, na maendeleo yaliyofikiwa katika kuchakata madini ya nickel hadi kufikia kiwango kinachoweza kutumiwa kuzalisha betri kwa ajili kutumika katika teknolojia ya nishati safi ni maendeleo makubwa sana. Kwa kusaini makubaliano ya Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania, kwa pamoja, tunapiga hatua nyingine kubwa katika kufikia kikamilifu uwezo huo.

 

Kwa mujibu wa makubaliano haya, Majadiliano ya Kibiashara yataongozwa kwa pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania na Waziri wa Biashara wa Marekani. Nchi zetu zitapokezana katika kuandaa mikutano ya kila mwaka ambayo washiriki wake watajumuisha maafisa waandamizi wa serikali za Marekani na Tanzania na viongozi wakuu wa wadau wa sekta binafsi. Katikati ya kila mkutano wa mwaka, wawakilishi wa Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam na wa Wizara ya Viwanda na Biashara watakutana mara kwa mara kuandaa mipango ya majadiliano, kutekeleza maamuzi, kushirikiana kupanga hatua zinazofuata, kubaini na kushughulikia masuala mbalimbali yanayokabili makampuni na kuwa wataalamu wa kiufundi ili kuzishauri serikali zetu mbili.  Majadiliano ya awali yatalenga katika uchumi wa kidijitali unaokua wa Tanzania, kuongeza uwezo wa kuyafikia masoko ya Marekani na Tanzania, mageuzi katika kanuni na mazingira ya kibiashara, kuandaa ziara za kibiashara kwenda Marekani na Tanzania, na kuandaa maonyesho ya kibiashara katika nchi zetu mbili.  Kwa pamoja, tutakuza maelewano yetu, tutajenga mahusiano mapya ya kibiashara baina ya nchi zetu, na kujifunza na kuchangia mbinu bora za utendaji katika kufanya kazi na masoko ya Marekani na Tanzania.

 

Baada ya muda, Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania yatakuwa msingi kwa ujenzi wa uhusiano rasmi wa kibiashara ulio imara na wa kudumu utakaowanufaisha wafanya biashara wa Marekani na Tanzania pamoja na raia wa kawaida wa nchi hizi. Iwe kwa kupeleka bidhaa bora za Kitanzania kwenye masoko ya Marekani au kwa kupanua ushiriki wa kiuchumi wa Marekani nchini Tanzania, kutengeneza nafasi za ajira zinazolipa vyema na kujenga tabaka la kati la Tanzania, makubaliano haya ni hatua ya kwanza.  Majadiliano endelevu kati ya serikali zetu na sekta zetu binafsi yatakuwa muhimu sana katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara, kuondoa vikwazo kwa biashara, kuunganisha chumi zetu, kutanzua masuala yanayokabili mnyororo wa ugavi na kufikia malengo yetu ya pamoja ya ustawi. Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania yakuwa jukwaa letu kufanya yote hayo na kuchambua kwa pamoja na kuimarisha sera za udhibiti zitakazowavutia wafanya biashara wa Kimarekani kuja Tanzania na wale wa Kitanzania Kwenda Marekani.  Wazalishaji, wenye viwanda, wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati wa Kitanzania wana nafasi kubwa zaidi ya kunufaika kutokana na majadiliano haya. Makubaliano hayo yatajenga mahusiano baina ya nchi zetu mbili yaliyo imara, endelevu na yenye manufaa kwa pande zote.

 

Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania ni hatua muhimu katika kufungua uwezo na fursa kubwa ya kiuchumi iliyopo katika ushirikiano rasmi kati ya Marekani na Tanzania. Serikali peke yake haiwezi kupanua fursa kwa raia wake kwa ukubwa sawa na ambavyo inaweza kuwa kwa kuishirikisha sekta binafsi. Tanzania ni nguvu ya kiuchumi na kinara katika Afrika Mashariki na bara zima. Marekani ni mbia aliyedhamiria kwa dhati kufikia matamanio yetu ya pamoja ya maendeleo ya kiuchumi na kwa pamoja tutaleta maendeleo makubwa yasiyo na mipaka.  Ni matarajio yangu kushiriki katika mkutano wa kwanza wa Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania na kuwakaribisha wabia wapya wa kibiashara wa Marekani katika soko hili zuri.