Wafanyakazi Wa Kujitolea Wa Peace Corps 55 Waapishwa Kuhudumu Katika Sekta Za Afya Na Kilimo

Wafanyakazi wa Kujitolewa wa Kimarekani kutoka shirika la Peace Corps wapatao 55 wamekula kiapo kuhudumu nchini Tanzania katika kipindi cha miaka miwili katika hafla iliyofanyika hivi leo katika Kituo cha Mafunzo kwa Wanawake cha Morogoro. Wafanyakazi hawa wa kujitolea watakaohudumu katika sekta za afya na kilimo watapangiwa kufanya kazi katika mikoa 20 nchini Tanzania.

Kiapo hicho rasmi kwa wafanyakazi hawa wapya wa kujitolea kiliendeshwa na Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps nchini Tanzania, Dk. Nelson Cronyn na kushuhudiwa na mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege.  Aidha, hafla hii ilihudhuriwa pia na taasisi nyingine washirika zinazojihusisha na wafanyakazi wa kujitolea na familia ambazo ziliwapokea na kuishi na wafanyakazi hawa wa kujitolea wakiwa katika mafunzo yao.

Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Tanzania aliielezea hafla hii kama tukio la kusherehekea dhamira ya dhati ya wafanyakazi wa kujitolea kuhudumu humu nchini na kielelezo cha ubia imara kati ya Tanzania na Marekani.  “Serikali ya Marekani inafanya kazi katika nyanja – kutoka masuala ya utawala hadi maendeleo ya kiuchumi na usalama wa kikanda – lakini kiini cha yale yote tunayofanya ni kuwasaidia watu wa Tanzania.  Tunafanya jambo hili vyema zaidi katika ngazi ya mtu na mtu. Hakika uhusiano kati ya wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps na familia zilizowapokea na wafanyakazi wenzao wa Kitanzania unafanya unadhihirisha maono hayo kwa vitendo kila siku,” alisema Cronyn.

Takriban wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps 3,000 wamehudumu nchini Tanzania toka mwaka 1962.  Peace Corps hutoa wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani wenye utaalamu katika nyanja mbalimbali ambao hupangiwa kufanyakazi katika jamii wakifundisha katika shule za sekondari (hisabati, sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano), wakitoa pia elimu ya afya na kilimo.

Wafanyakazi wa kujitolea hutoa usaidizi na mafunzo katika elimu ya mazingira ikiwa ni pamoja kusaidia jitihada za kuzuia uharibifu wa ardhi, uhifadhi wa vyanzo vya maji, uhifadhi wa ardhi na utekelezaji wa mbinu bora za uzalishaji wa kilimo na misitu huku wakiweka msisitizo katika ushiriki wa wanawake na vijana. Pia watatoa mafunzo na kuwezesha kuanzishwa kwa kilimo hai cha bustani (bio-intensive gardens) ili kuongeza upatikanaji wa chakula, na kuboresha lishe ya kaya pamoja na shughuli nyingine za kujiongezea kipato.

Aidha, wafanyakazi hawa wa kujitolea husaidia katika kuimarisha afya ya umma kwa kufanya kazi na vituo, vikundi vya kijamii na vile vilivyomo mashuleni vinavyotoa huduma na elimu ya afya ikiwa ni pamoja na zile zinazohusu kujikinga dhidi ya VVU/UKIMWI, matibabu na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI,yatima na watoto walio katika mazingira hatarishi. Wafanyakazi wa kujitolea hufanya kazi kwa karibu na kamati za afya vijiji ili kubaini na kuchambua mahitaji na vipaumbele vya jamii na kushiriki katika shughuli zinazohamasisha mabadiliko ya tabia katika maeneo ya afya ya mama na mtoto, lishe, malaria, maradhi yanayosababishwa na maji yasiyo salama, afya ya uzazi na kinga dhidi ya VVU/UKIMWI.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.