Flag

An official website of the United States government

3 MINUTE READ
Febuari 21, 2023

Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps Warejea Tanzania

Dar es Salaam – Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani wa Peace Corps jana wamerejea nchini Tanzania baada ya kutokuwepo nchini kwa takriban miaka mitatu. Wafanyakazi wa kujitolea 18 waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 19 Februari, wakiwa ni kundi la kwanza kurejea Tanzania toka kuzuka kwa janga la UVIKO-19, mwezi Machi 2020 lililolazimisha kurejeshwa nyumbani kwa zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 7,000 kutoka maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo 158 kutoka Tanzania.

 

Kabla ya kurejeshwa nyumbani, Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps walikuwa wamehudumu nchini Tanzania kwa zaidi ya miongo sita. Kutoka Septemba 1961 hadi Machi 2020, zaidi ya Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps 3200 walikuwa wamehudumu nchini Tanzania, wakifanya kazi katika sekta za elimu, kilimo na afya wakishughulikia vipaumbele muhimu vya maendeleo na wakati huo huo wakikuza amani ya dunia na urafiki. “Kutokana na uhusiano huu wa kina, kurejea kwa wafanyakazi hawa wa kujitolea nchini Tanzania baada ya kutokuwepo nchini kwa miaka mitatu ni jambo linalostahili kusherehekewa,” alisema Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Tanzania Stephanie Joseph de Goes.

 

“Ninaishukuru serikali ya Tanzania, na jamii washirika kwa kuipokea Peace Corps. Ni heshima kubwa kwetu kufanya kazi na watu waliojitoa kwa dhati katika nchi hii nzuri. Toka mwezi Machi 2020, wafanyakazi wa Peace Corps duniani kote wamekuwa wakifanya kazi ya kuimarisha misingi ya taasisi yetu. Sasa tupo tayari kuzindua tena huduma ya wafanyakazi wa kujitolea na kuadhimisha wakati huu wa kihistoria pamoja na jamii washirika wetu na wafanyakazi wetu wa Peace Corps.”

 

Baada ya mafunzo ya wiki 11 yatakayojumuisha mafunzo ya lugha ya Kiswahili, utamaduni wa Kitanzania na ujuzi mahsusi wa kiufundi kulingana na sekta zao, wakufunzi hao wataapishwa kuwa Wafanyakazi wa Kujitolea ili kuanza miezi yao 24 ya utoaji huduma.  Kwa maombi ya Serikali ya Tanzania, wafanyakazi wapya wa kujitolea wataelekezwa katika sekta ya elimu watakapofundisha masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) katika shule za sekondari, Kilimo Endelevu na Elimu ya Afya ya Jamii. Hali kadhalika, wafanyakazi wote wa kujitolea watajumuisha suala la kuzuia maradhi (VVU, malaria na UVIKO) katika huduma watakazotoa pamoja na suala la mabadiliko ya tabia nchi na shughuli zinazowalenga vijana.

 

Kuhusu Peace Corps:  Peace Corps ni mtandao wa kimataifa wa huduma wa wafanyakazi wa kujitolea , wanajamii, wabia katika nchi wenyeji na wafanyakazi wanaosukumwa na lengo la shirika hili la kujenga amani duniani na urafiki. Kwa mwaliko wa serikali wenyeji, wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps hufanya kazi na wanajamii wa jamii husika katika miradi ya kipaumbele ya jamii zenyewe katika nyanja za elimu, afya, mazingira, kilimo, uchumi, maendeleo ya jamii na maendeleo ya vijana. Kupitia huduma hizi wanachama wa mtandao wa Peace Corps hupata stadi mbalimbali pamoja na ujuzi wa kuweza kufanya kazi na watu wa tamaduni tofauti (intercultural competencies) unaowaweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuwa kizazi kijacho cha viongozi wa kimataifa. Toka mwaka 1961 pale Rais John F. Kennedy alipoanzisha Peace Corps, zaidi ya Wamarekani 240,000 wamehudumu kama wafanyakazi wa kujitolea katika nchi 142 duniani kote.