Flag

An official website of the United States government

Wafanyakazi wapya 21 wa Kujitolea wa Peace Corps waapishwa kuanza huduma yao Tanzania
4 MINUTE READ
Disemba 7, 2023

Dar es Salaam, TANZANIA – Leo, katika hafla fupi iliyofanyika katika makao makuu ya Peace Corps Tanzania, Wamarekani 21 wameapishwa kuwa Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps. Hafla hiyo iliongozwa na Balozi Michael Battle na Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Tanzania Stephanie Joseph de Goes.

Katika kuenzi urithi tulioachiwa na Mwalimu Julius Nyerere na John F.Kennedy wa kujitoa kwajili ya amani na urafiki duniani,wafanyakazi wapya wa kujitolea wa Peace Corps wanaungana na makada zaidi ya 3200 wake kwa waume waliohudumu Tanzania tangu kuanza kwa program hii 1961.

Baada ya wiki 12 za mafunzo ya kina ya lugha ya Kiswahili, utamaduni, ulinzi na usalama, afya na ujuzi mahsusi wa sekta katika kukabili na kutoa ujuzi kwa jamii, wafanyakazi hawa wapya wapo tayari kuanza kazi katika vituo vyao vya kazi katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro na Tanga. Wafanyakazi hawa wataishi na kufanyakazi kwa miaka miwili kwenye eneo la elimu ya sekondari kwa masomo ya Hisabati na Sayansi, eneo la afya ya Jamii, Kilimo endelevu kinachohusisha  ukuzaji wa ustahimilivu wa hali ya hewa.

Katika hotuba yake kabla ya kusimamia kiapo kwa wafanyakazi wapya wa kujitolea, Balozi Battle aliwaeleza wafanyakazi hao, “Kumbuka uwepo wako na kufanya kazi katika jamii za Kitanzania kutatoa dirisha kwa jamii ya Wamarekani na utamaduni. Mimi ni balozi wa Marekani nchini Tanzania lakini kila mmoja wenu ni balozi katika upande wake.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps nchini Tanzania Stephanie Joseph de Goes alisisitiza nguvu ya kujitolea katika kukuza matendo jumuishi ya kusaidia jamii zetu na dunia yetu. Alitoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania na familia zilizoishi na wafanyakazi wa kujitolea kwa kuisaidia Peace Corps kuwapokea na kutoa mafunzo. Alisisitiza dhamira ya dhati ya Peace Corps kufanya kazi na Tanzania kwa moyo wa ushirikiano, unyenyekevu na heshima.

Kuhusu Peace Corps:  Peace Corps ni mtandao kimataifa wa wafanyakazi wa kujitolea, wanajamii, wabia wa nchi zinazowapokea wafanyakazi hao na wafanyakazi wanaosukumwa na dhima ya shirika ya kuwa na dunia yenye amani na urafiki. Kwa mwaliko wa serikali mbalimbali duniani kote, wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps hufanya kazi na wanajamii wa jamii husika katika miradi yao ya kipaumbele katika maeneo ya elimu, afya, mazingira, kilimo, maendeleo ya kiuchumi ya jamii na maendeleo ya vijana. Kupitia huduma hii, wafanyakazi wa kujitolea na wale wote walio katika mtandao wa Peace Corps hujenga stadi mbalimbali wanazoweza kuzitumia mahali pengine na ujuzi wa kufanya kazi na watu wa tamaduni tofauti tofauti hivyo kuwaweka katika nafasi nzuri ya kuwa kizazi kijacho cha viongozi wa kimataifa. Toka Rais John F. Kennedy alipoanzisha Peace Corps mwaka 1961, zaidi ya Wamarekani 240,000 wamehudumu katika nchi 142 duniani kote. Zaidi ya Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps 3200 wamehudumu nchini Tanzania toka programu hii ilipoanza mwaka 1961, wakifanyakazi katika sekta za elimu, kilimo na afya, wakishughulikia vipaumbele muhimu vya maendeleo na wakati huo huo wakikuza amani na urafiki duniani.