Warsha ya Muziki na Ujasiriamali kwa wanamuziki wa Kitanzania

Muziki ni furaha, muziki ni burudani, muziki ni njia ya kueleza hisia, muziki ni nyenzo muhimu ya kuelimisha, kuonya, kuelekeza na kuihamasisha jamii katika masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na hata kiimani.  Toka enzi na enzi, muziki umekuwa si tu kielelezo cha tamaduni za binadamu, bali pia nyenzo ambayo binadamu anaitumia kurithisha utamaduni, desturi na hata maarifa yake kwa vizazi vijavyo.  Mwanamuziki na msanii mahiri, Dr. Remmy Ongala, Mungu amrehemu, katika kibao chake murua “Muziki asili yake wapi?”alitukumbusha haya yote na kutufunza kwamba muziki ni maisha.

Kwa upande mwingine, muziki ni taaluma, muziki ni kazi na muziki ni biashara. Kwa maana hiyo, kama zilivyo taaluma, kazi na biashara nyingine zote, muziki ni chanzo cha mapato na uchumi.

Taarifa rasmi iliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali  inaonyesha kuwa sekta inayoongoza kwa kuupaisha uchumi wa nchi ni ile ya sanaa na burudani ambayo ilikua kwa asilimia 13.7 ikipiku kasi ya ukuaji wa sekta nyingine ikiwemo sekta za ujenzi (asilimia 12.9), usafirishaji (asilimia 11.8), sayansi na elimu ya ufundi (asilimia 9.9) na hata habari na mawasiliano (asilimia 9.1).  Je wasanii, hususan walio katika fani ya muziki, wanatambua na kunufaika kikamilifu kutokana na nguvu hii kubwa ya kiuchumi waliyonayo? Wanaziona fursa? Wanazitumia? Ni wazi kuwa kwa kutokuziona na kuzitumia fursa hizo kikamilifu, wanamuziki, kama walivyo wanajamii wengine wasioweza kuona fursa mbalimbali zinazowazunguka wataendelea kutumika kama nyenzo za kuwanufaisha na kuwatajirisha wengine.

Hivi karibuni, wanamuziki vijana na viongozi wa vikundi vya wanamuziki wapatao 25 kutoka sehemu mbalimbali nchini, walishiriki katika warsha maalumu ya siku mbili kuhusu muziki na ujasiriamali iliyofanyika katika kituo cha uendelezaji Sanaa cha Nafasi Art Space. Warsha iliandaliwa na Nafasi Art Space na kufadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wake jijini Dar es Salaam chini ya programu yake ya mabadilishano ya kitamaduni.

Akielezea sababu za kuandaa warsha hii, meneja wa maonyesho ya Jukwaani wa Nafasi Art Space Kwame Mchauru alisema “uzoefu wetu unaonyesha kuwa hivi sasa kuna wasanii wengi wanaochipukia lakini hawana taaluma rasmi ya kuendeleza vipaji vyao na hata namna ya kuendesha shughuli zao kwa ufanisi. Hali kadhalika, hapa nchini hakuna watu wengi wenye utaalamu katika kada ya usimamizi wa Sanaa na wasanii (Arts Management). Kutokana na hali hiyo, wasanii wengi hubaki wakihangaika kufanya kazi zao za kisanii huku wakisimamia wenyewe masuala ya kimenejimenti ikiwemo usimamizi wa mapato na matumizi. Warsha hii itawasaidia sana wasanii wetu na viongozi wa vikundi vyao kujua namna ya kujisimamia kifedha na kujiendeleza kiuchumi”

Kwa upande wake, Afisa Msaidizi anayeshughulikia masuala ya utamaduni katika Ubalozi wa Marekani Bi. Mariya Boston alisema kuwa warsha hii inakwenda sambamba na lengo la ubalozi huo la kuwajengea uwezo wa kiuchumi Watanzania, hususan vijana wa Kitanzania, ikiwemo kupitia Sanaa ya muziki ambayo wanaipenda sana. “Isitoshe hii ni fursa mojawapo yenye ufanisi ya kuimarisha ushirikiano baina ya watu wa nchi zetu mbili,” alisema Bi. Boston.

Mwezeshaji mkuu wa warsha hii alikuwa ni Mwanamuziki wa Kimarekani Kenny Wesley, aliyeshirikiana na wenzake wanne, Zachary Cutler, Christopher Bynum, Dennis Turner na Alexander Joseph. Kenny ambaye ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Howard nchini Marekani ambako anafundisha Kifaransa na Kihispania, alianza rasmi muziki akiwa na miaka saba na amedumu katika tasnia hiyo kwa zaidi ya miaka 30.

Miongoni mwa mada kuu zilizojadiliwa katika warsha hii iliyoendeshwa zaidi kwa mbinu shirikishi ya kubadilishana uzoefu, zilikuwa ni pamoja na namna ya kufanya muziki kama kazi na kujiendeleza kama mwanamuziki mwenye weledi, haiba na mienendo  sahihi (Career Development), umuhimu wa kujenga na kuimarisha ushirikiano na wadau muhimu watakaoweza kumsaidia msanii kupata maendeleo katika fani yake na maendeleo ya kiuchumi na jinsi ya kujenga mitandao yenye ufanisi miongoni mwa wasanii. Mada nyingine zilizojadiliwa ni jinsi ya kuchambua soko la muziki, jinsi ya kuwa mwanamuziki anayetengeneza kipato na faida katika kazi yake na vyanzo mbalimbali vya mapato kwa wasanii.

Mojawapo ya mada ziliyojadiliwa kwa msisimko mkubwa ilikuwa ni ile ya kutumia mitandao ya kijamii kama fursa ya kiuchumi. Kimsingi washiriki walishauriwa kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, wakitenganisha maisha yao binafsi na shughuli zao za kikazi. Aidha, walipewa mbinu za kuwafikia watu wengi zaidi watakaoweza kuwainua kiuchumi na kisanii kupitia mitandao ya kijamii. Ilielezwa kuwa kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujenga umaarufu pekee bila kuifanya kama chombo cha kimkakati cha kuzalisha kipato na kuongeza ujuzi hakutaweza kumkomboa msaanii kiuchumi.

Mwezeshaji mkuu Kenny Wesley alielezea kufurahishwa kwake na kiwango cha juu cha ubunifu alichokishuhudia miongoni mwa washiriki wa warsha na kusema kuwa wanachohitaji sasa ni kupanua wigo wa kazi zao ili kufikia ngazi za kimataifa. “Wanahitaji kupanua mawazo yao na kutumia fursa mbalimbali za kujitangaza kimataifa, hususan, kupitia mitandao mbalimbali ya kjjamii inayoweza kufikisha kazi zao katika majukwaa ya kimataifa,” alisema.

Mmoja wa washiriki wa warsha, Anette Ngongi a.k.a Seghito anayefanya muziki wa soul, blues, Jazz na midundo ya Kiafrika anasema kuwa jambo kubwa alilojifunza katika warsha hii ni namna ya kujenga uhusiano na wasanii wengine pamoja na namna ya kuuvusha muziki wake nje ya mipaka ya Tanzania.

Mshiriki mwingine Halima Ramadhani anayefanya muziki wa Singeli anasema kuwa kwa mara ya kwanza amepata mwanga wa namna anavyoweza kufanya shughuli za muziki na kunufaika kiuchumi pamoja na kuongeza idadi na ukubwa wa vyanzo vyake vya mapato.

Baada ya warsha, wawezeshaji na washiriki walijumuika pamoja kupiga muziki uliochanganya vionjo vya Kimarekani na Kitanzania ikiwemo muziki maarufu wa Singeli. Hakika muziki ni lugha ya kimataifa iwezayo kuvunja mipaka ya kila aina.