Watuhumiwa Watatu Wa Usafirishaji Wa Madawa Ya Kulevya Wasafirishwa Kwenda Marekani

Kutokana Na Ushirikiano Imara Wa Kiusalama Kati Ya Marekani Na Tanzania

Dar es Salaam, TANZANIA. Hapo tarehe 1 Mei 2017, mtuhumiwa wa usafirishaji wa madawa ya kulevya Ali Khatib Haji Hassan (“Shkuba”) na washirika wake wawili Iddy Salehe Mfullu na Tiko Emanual Adam walisafirishwa kwenda nchini Marekani, kukabili mashtaka yao kuhusiana na biashara haramu ya madawa ya kulevya katika Mahakama kuu huko Huston, Texas. Watuhumiwa hao watatu waliwasili nchini Marekani tarehe 2 Mei 2017. Kusafirishwa kwa watuhumiwa hao ni matokeo ya ushirikiano mkubwa, wa karibu na wa muda mrefu baina ya serikali za Marekani na Tanzania.

“Kupelekwa nchini Marekani kwa Hassan na washirika wake ni mafanikio yatokanayo na ushirikiano wetu wa muda mrefu na wenzetu katika serikali ya Tanzania katika nyanja nyingi katika sekta za usalama, usimamizi wa sheria na haki. Kesi hii ni mfano mzuri sana wa jinsi tunavyoweza kuimarisha usalama wa kikanda na kimataifa pale tunapofanya kazi pamoja,” alisema Virginia Blaser, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mamlaka za Tanzania zilimtia mbaroni Shkuba kwa tuhuma za usafirishaji madawa ya kulevya hapo mwaka 2014 baada ya msako wa miaka miwili uliofuatia kukamatwa kwa takriban kilo 210 za dawa za kulevya aina ya heroine huko Lindi Tanzania mwezi Januari 2012. Tarehe 9 Machi 2016, Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni ya Wizara ya Fedha ya Marekani (U.S. Department of the Treasury’s Office of Foreign Assets Control – OFAC) chini ya sheria ya kuwabainisha raia wa kigeni walio vinara wa biashara ya madawa ya kulevya (Foreign Narcotics Kingpin Designation Act – Kingpin Act) ilimtaja Hassan na kundi lake kama raia wa kigeni aliye kinara wa biashara hiyo haramu. Kwa taarifa zaidi kuhusu tamko hilo la OFAC, tembelea https://www.treasury.gov/press-center/press-releases/Pages/jl0378.aspx

Mwezi Machi 2016, Jopo la maafisa mashtaka (grand jury) la Huston, Texas, lilipitisha mashtaka dhidi ya Shkuba na washirika wake kwa tuhuma za kula njama ya kumiliki kwa lengo la kusambaza madawa ya kulevya aina ya heroin nchini Marekani katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2015. Hatimaye serikali ya Marekani iliwasilisha ombi rasmi kwa Tanzania la kuwapeleka watuhumiwa hao watatu nchini Marekani.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.